HomeResourcesSabbath School quarterly
Eliya — Kuomba katika Zahama
10/05/2026
Eliya aliyekuwa mwaminifu aliishi zama za uovu, wakati mfalme Ahabu akazidi “kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia” (1 Fal. 16:33). Wakati wa ajabu kupita zingine zote katika maisha ya Eliya ulikuwa wa makabiliano katika Mlima Karmeli (taz. 1 Fal. 18). Katika kilele cha kisa hiki cha kustaajabisha, Ahabu na ufalme wake waliona kwa macho yao wenyewe ukweli kwamba Mungu hujibu maombi. Huu ulikuwa wasaa usioweza kusahaulika katika historia ya Waisraeli na ndio maana badiliko la ghafla la matukio katika kisa hiki yanatustaajabisha
Ndani ya siku moja, ingawa Mungu alijibu kila moja ya maombi ya Eliya, hali ya kihisia, kiakili na kimwili ya Nabii ilibadilika mara. Ingawa Eliya alikuwa amepata uzoefu wa ushindi mkuu pamoja na Mungu siku ile, alikuwa, katika saa ya uchovu ameruhusu hofu ya kifo kuishinda imani yake kwa Mungu. Kinachoshangaza zaidi juu ya kisa hiki ni kwamba ingawa Eliya alijisalimisha katika kukata tamaa na kuvunjika moyo, Mungu alimjia kwa huruma na upole, akimpatia chakula na maji tena (1 Fal. 19:5, 6) — kiasi kwamba alikaa bila kula tena kwa siku 40 usiku na mchana (1 Fal 19:8). Na wakati ambapo hatimaye Mungu Alijifunua, ilikuwa kwa namna tofauti kabisa na hapo kabla.
Nyakati zingine katika maisha yetu, Mungu hujibu kwa namna ya moja kwa moja, yenye nguvu, na isiyopingika. Hii huimarisha imani yetu, nasi tunahisi ukaribu wa Mungu katika maisha yetu.
Nyakati zingine tunayumba na kujisalimisha katika majaribu, tukidhani kwamba ni jambo gumu mno kumfuata Mungu kwa imani isiyoyumba. Tunatafuta majibu ya Mungu kwa njia tunazomtarajia ajibu, bila kutambua kwamba njia Zake na mawazo Yake ni ya juu mno na ya hekima mno kuliko vyetu (Isaya 55:8, 9). Kama ambavyo kuna mengi kuhusiana na uumbaji wa Mungu tusiyoyajua, tusishangae kwamba kuna mengi kuhusiana na njia za Mungu ambayo hatuyajui pia.