HomeResourcesSabbath School quarterly

Kusifu, Ungamo, Mahitaji, Kushukuru

13/05/2026

Kwa jinsi ile ile ambayo Yesu alitufundisha kusali katika Mathayo 6:5-15, tunaweza kufuata kielelezo hiki rahisi tunapokuja kwa Mungu kwa faragha, pamoja na familia zetu au kama kanisa, tukikumbuka kuwa maombi ni kuzungumza na Mungu kama kuzungumza na rafiki. Mara nyingi maombi yetu yamejaa haja zetu ingawa Yesu ametufundisha kuomba kwa ajili ya mengi zaidi ya hayo.

Zingatia jinsi unavyoweza kujumuisha vipengele vifuatavyo katika maombi yako:

Kusifu: ni kuonesha sifa na ibada kwa sababu ya Yeye ni nani na vile alivyo. Soma Zaburi 100, wimbo mzuri wa sifa kwa Mungu. Angalia majina mengi ya Mungu, na tabia Yake iliyotukuka. Msifu kwa kuwa Mkombozi, Mwokozi, Mfariji, Mponyaji, Mchungaji Mwema, Alfa na Omega na Mwamba, hivi ni vichache kati ya vingi.

Ungamo na Msamaha: Tunapojikuta tukiongea na Mungu na kukaa ndani Yake, ni lazima tu tutaachilia chochote kinachotuzuia au kututenga Naye. Kadiri tunavyokuwa karibu zaidi Naye, ndivyo tunavyozidi kuona kutostahili kwetu na umaskini wetu. Hii inatufanya tumsihi Aondoe dhambi zetu na kuitengeneza tabia yetu ili ifanane Naye. Ikiwa tunataka Mungu atusamehe, ni lazima tuwe tayari kuwasamehe wengine pia. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii” (Yak. 5:16).

Mahitaji: Ni changamoto gani unakabiliana nazo, bila shaka na familia yako, marafiki, afya, fedha, kazi, au masomo? Ni wapi hasa unahitaji mkono wa Mungu ukuongoze? Ni nani anahitaji msaada wako, na ni kwa njia zipi bora unaweza kuutoa? Omba mahususi kwa ajili ya maeneo hayo na watu ukiomba mapenzi ya Mungu yatimizwe.

Kushukuru: Soma Wafilipi 4:6 kisha utafakari juu ya mibaraka ya Mungu maishani mwako. Utaweza kukumbuka vitu muhimu, lakini vipi kuhusu vitu vidogo ambavyo mara nyingi hatuvizingatii? Sisi ni wapokeaji wa daima wa rehema za Mungu; na bado ni shukrani Kidogo kiasi gani huwa tunatoa, ni kiasi kidogo sana tunamsifu kwa ajili ya kile alichotutendea.