HomeResourcesSabbath School quarterly

Hatimaye, Ana kwa Ana

22/06/2026

Tuliumbwa tuwe karibu na Mungu (Mwa. 2:7). Tangu alipoumba jamii ya wanadamu, Mungu ametoa kila kitu ili kurejesha uhusiano uliovunjika kati yetu na Yeye (Yn. 3:16). Ameweka milele ndani ya mioyo yetu, licha ya hivyo wanadamu hawawezi kuelewa kile Mungu alichofanya tangu mwanzo hadi mwisho (Omb. 3:11). Sisi ni sehemu ya pambano kuu linalozidi kote kutuzunguka — hata ndani yetu — hata hivyo, mara nyingi huwa hatutulii kiasi cha kutosha kutafakari gharama kubwa ya kile ambacho kimetolewa ili tupate kurejeshwa kwenye uhusiano ambao Mungu ameukusudia kwamba sisi tuwe nao pamoja Naye. Mara nyingi sana, tunajikuta tukiwa tumezingwa katika mapambano na majaribu yetu ya kidunia, tukisahau kwamba wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo (Flp. 3:20,21).

Ulimwengu unapoporomoka ukikaribia mwisho, tunajua kwamba wingu dogo jeusi, siku moja litatokea kwenye anga la mashariki. Litakapokuwa likisogea karibu zaidi na zaidi, tutaona kwamba kwenye wingu lile atakuwa ameketi mmoja, mfano wa Mwanadamu, mwenye taji ya dhahabu juu ya kichwa chake, na katika mkono wake mundu mkali (Ufu. 14:14). Bwana Yesu atasindikizwa na maelfu kwa maelfu ya malaika (Mt. 25:31) na kila jicho litamwona (Ufu. 1:7). Atakapokuwa akishuka, tutasikia kelele yake, mwito wa tarumbeta ya Mungu, na makaburi ya wale waliolala katika Kristo yatafunguka watakapokuwa wakiinuka kwanza (1 The 4:16). Wataijua sauti Yake atakayekuwa akiwaita (Yn. 5:28).

Ni wazo zuri la kushangaza kiasi gani! Siku moja tutamwona Bwana Yesu — kweli kweli, tutamwona Yeye. Tutaisikia sauti Yake, nasi tutakiri kwamba Yeye ni Bwana, Yeye ambaye tumesoma habari zake, ambaye tumekuwa tukimwomba, ambaye tumekuwa tukimzungumza kwa wengine; Yeye ambaye mioyo yetu imekuwa na shauku juu yake…. Kwa kweli tutamwona uso kwa uso. Tunaweza kuwa na hakika juu ya hili, kwani Mungu ni mwaminifu na ahadi Zake ni za kweli (Ufu. 22:6).

Wakati huo, pale tarumbeta itakapolia na jicho la kila mtu litakapomwona Yesu, tutajua kwamba kusubiri kwetu kumekuwa kwa maana. Kila ombi la uvumilivu, kila fursa ambayo tumeipa kipaumbele ya kuwa Naye, kila muda ambao tumeutumia kunena kwa ujasiri kwa ajili Yake, kila jaribu — litahitimishwa kwa kuuona uso Wake (Ufu. 22:4)