HomeResourcesSabbath School quarterly

Njoo!

25/06/2026

Umepewa mwaliko tena leo: Njoo.

Roho Mtakatifu anataka kukuvuta kwa Yesu leo. Yesu anakualika uje Kwake, kukaa ndani Yake leo na kila siku, hadi atakapokuja. Wakati unapomwitikia na kumjia Yeye, wakati moyo wako ni laini na nia yako ikiwa imesalimishwa, utajisikia amani kwa sababu ya kujua kwamba atakuinua, licha ya jinsi unavyoweza kujisikia kutokufaa, katika siku ya mwisho wa dunia hii. Yesu alisema, Ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe (Yohana 6:37).

Tunapaswa kuhisi umuhimu wa kufanya kazi na Roho Mtakatifu kuwaita wengine ili waingie katika uhusiano unaookoa na Yesu. Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure (Ufu. 22:17).

Mwaliko ni bure, unaotolewa kama zawadi ya neema. Tunapomkubali maishani mwetu na kumpenda kwa mioyo yetu yote, akili zote, roho zetu na nguvu zetu zote (Kum. 6:5), maisha yetu hapa na ya wakati ujao yatabadilishwa milele.

Bwana Yesu anapotualika tumjie Yeye, maneno ya mwisho katika Biblia yanaahidi hivi: Naam; naja upesi. Amina; na uje, Bwana Yesu. (Ufu. 22:20, mkazo umeongezwa).

Upesi kiasi gani? Kwa mtazamo wetu, mara tu tunapofunga macho yetu tukifa, jambo linalofuata tunalojua litakuwa ni kurudi kwa Kristo. Tukizingatia jinsi maisha yetu yanavyopita upesi, ndivyo Yesu anavyorudi kwa upesi. Pengine wazo letu la kwanza tukifufuka litakuwa Wauu, Bwana, ujio wako umefika upesi sana!

Kwa kweli, sasa tunaona lakini kwa namna hafifu, kama kwenye kioo. Lakini wakati huo tutamwona ana kwa ana. Usichoke katika kusubiri. Dumisha uhai wa shauku hii daima mbele yako, kwa imani na katika tumaini katika upendo na wema wa Mungu. Bwana Yesu, tafadhali njoo upesi!