HomeResourcesSabbath School quarterly
Dhoruba za Maisha
07/06/2026
Yesu alikuwa ameitumia siku akihubiri kwa makundi makubwa ya watu katika pwani za Galilaya. Maneno Yake yangekumbukwa kwa muda mrefu katika akili za watu na hata milele.
Jioni ilipowadia, Yesu akazungumza na wanafunzi Wake, akiwakaribisha katika safari pamoja Naye: “Na tuvuke mpaka ngambo” (Marko 4:35). Yesu alijua dhoruba ingekuja, lakini bado akapendekeza waende. Alikuwa na somo muhimu la maisha alilotaka kuwafundisha wafuasi Wake wa karibu.
Bila shaka unajua kilichotokea.
Zingatia hoja hizi:
- Yesu analala usingizi juu ya kile kinachoonekana kuwa mto pekee katika mashua. Mashua za uvuvi kwa kawaida zilikuwa na mto mmoja, ambao dereva wa mashua, katika shetri, alikalia. Mtu aliyekuwa katika shetri ndiye aliyekuwa akiielekeza mashua kufika ilikokusudiwa. Hivyo basi, Yesu yuko katika nafasi ya “dereva” wa mashua, lakini analala akiwa kwenye usukani.
- Si wanafunzi wote walikuwa wapya katika masuala ya kusafiri baharini. Petro, Yakobo, na Yohana walikuwa wavuvi wenye uzoefu. Waliijua bahari ya Galilaya, na wangekuwa wanajua jinsi ya kuongoza mashua wakati wa dhoruba.
- Hii ndiyo simulizi pekee katika Injili inayoandikwa juu ya kulala usingizi kwa Yesu. Wakati wa moja ya dhoruba mbaya zaidi katika maisha yao, wanafunzi walipokuwa na hofu na wakidhani wangekufa, Yesu alikuwa amelala katika shetri.
- Mwitikio wa wanafunzi wakati wa dhiki yao ulikuwa “si kitu kwako kuwa tunaangamia? Walihoji tabia ya Yesu na upendo Wake kwao. Mara nyingi, huu ndiyo mwitikio wetu tunapokumbana na nyakati ngumu.
Ni katikati ya hali ya kukata tamaa ndipo tunaweza kujaribu kujiokoa wenyewe (kama wanafunzi), au wakati mwingine ni tunapohisi maumivu au kupoteza ndipo tunapoanza kuhoji au kutilia shaka upendo na utunzaji wa Mungu kwetu. Tunadhani kwamba Yeye anapaswa kutenda kwa namna fulani kulingana na tunavyofikiri na kuona kutoka katika mtazamo wetu wa kibinadamu. Lakini, kama ilivyokuwa kwa wanafunzi, ni katika dhoruba za maisha ndipo Mungu anaweza kufanya miujiza mikubwa zaidi. Mungu ni mwaminifu kila wakati, hata pale ambapo kutokuwapo kwake kwa dhahiri hakueleweki kwetu. Yuko pamoja nasi katika dhoruba zetu na anaweza kuituliza dhoruba pale ambapo sisi hatuwezi.