HomeResourcesSabbath School quarterly

Mtazame Yesu

11/06/2026

Je, umewahi kutamani kumwona Yesu unapohisi kukatishwa tamaa? Jitazame katika ndoto hii. “Nilionekana kuketi katika hali ya kukata tamaa kabisa, mikono ikiwa usoni mwangu, nikitafakari hivi: Kama Yesu angekuwa duniani, ningemwendea, nianguke miguuni Mwake, na nimweleze mateso yangu yote. Asingenikataa, ningepata neema machoni Pake, nami ningempenda na kumtumikia daima. Wakati huo huo mlango ukafunguka, na mtu mwenye umbo na uso wa kupendeza akaingia. Alinitazama kwa huruma na kusema: “Je, unatamani kumwona Yesu? Yuko hapa na unaweza kumwona ikiwa unatamani kufanya hivyo. Chukua kila kitu ulicho nacho na unifuate.”

“Nilisikia jambo hili kwa furaha isiyoelezeka, na kwa furaha nikakusanya kila kilicho changu, kila kitu kidogo kilichokuwa cha thamani, na kumfuata kiongozi wangu. Aliniongoza hadi kwenye ngazi iliyoinuka na iliyokuwa dhaifu kwa kuonekana. Nilipoanza kupanda ngazi hizo, alinitahadharisha kukaza macho yangu juu daima, nisije nikapata kizunguzungu na kuanguka. Wengi waliokuwa wakipanda ngazi hiyo walianguka kabla ya kufika kileleni

Hatimaye tukafika kwenye ngazi ya mwisho na kusimama mbele ya mlango. Hapa kiongozi wangu alinielekeza niache kila kitu nilichokuwa nimebeba. Kwa furaha nikaviweka chini; kisha akaufungua mlango na kuniambia niingie. Kufumba na kufumbua nikajikuta nimesimama mbele ya Yesu. Hakukuwa na shaka juu ya uso huo mzuri. Mwangaza wa rehema na ukuu uliokuwa ukimng’aria usingeweza kuwa wa mtu mwingine yeyote. Macho Yake yaliponitazama, nilijua mara moja kwamba alikuwa anafahamu kila hali ya maisha yangu na kila wazo na hisia ya ndani ya moyo wangu.

“Nilijaribu kujificha dhidi ya macho Yake, nikihisi kushindwa kustahimili macho Yake yachunguzayo, lakini alinikaribia kwa tabasamu, na akaweka mkono Wake juu ya kichwa changu, akasema: ‘Usiogope.’ Sauti Yake tamu ilisisimua moyo wangu kwa furaha ambayo sikuwahi kuipata kabla. Nilijawa na furaha kiasi kwamba sikuweza kusema neno lolote, bali kwa kushindwa kustahimili furaha isiyoelezeka, nilianguka kifudifudi miguuni Mwake. Nilipokuwa nimelala pale bila kujiweza, mandhari ya uzuri na utukufu ilipita mbele yangu, na nikahisi kana kwamba nimefikia usalama na amani ya mbinguni. Hatimaye nguvu zangu zikarudi, nikainuka. Macho ya upendo ya Yesu bado yalikuwa juu yangu na tabasamu Lake lilijaza roho yangu kwa furaha. Uwepo Wake ulijaza moyo wangu kwa heshima kuu na upendo usioelezeka.

“Ndoto hii ilinipa tumaini... [na] imani.... Na uzuri na urahisi wa kumtumaini Mungu ulianza kuchomoza katika roho yangu iliyokuwa gizani.”—Ellen G. White, Early Writings, uk. 79-81.

Katikati ya changamoto za maisha, tunapaswa kukaza macho yetu kwa Yesu na kile Anachofunua kuhusu upendo wa Mungu kwetu.