HomeResourcesSabbath School quarterly

Njia kwenda Emau

10/06/2026

Yalikuwa majuma machache mazito kwa wale wanafunzi wawili walipokuwa wakikumbuka katika akili zao baadhi ya matukio na mazungumzo waliyopitia. Kuingia kwa ushindi Yerusalemu na kutakasa hekalu. Pasaka katika chumba cha juu. Maombi ya Yesu kule Gethsemane. Usaliti mbaya wa Yuda. Shitaka, dhihaka, na kupigwa. Mwili wa Yesu uliokuwa umejeruhiwa ukining'inia msalabani na maneno Yake ya mwisho kabla hajakata roho huku anga la alasiri likifunikwa kwa giza. Kupasuka kwa pazia la hekalu kwa sauti kubwa. Makaburi ya wenye haki yakifunguka, Kuchukua kwa upole mwili wa Yesu kutoka msalabani na kuuweka kaburini kabla ya Sabato. Na kisha machafuko, kukatishwa tamaa, na maswali katika akili za wanafunzi. Walikosea wapi?

Wafuasi wa Yesu walikuwa wamevunjika moyo, wamekata tamaa, na kuchanganyikiwa. Hili lilikuwa pigo kubwa zaidi katika maisha yao. Kile Ambacho hawakuona ni kwamba hili lilikuwa tu tukio moja katika kisa adhimu zaidi kuwahi kutokea. Wakati wawili wao walipokuwa wakitembea katika njia ya kuelekea Emau, Yesu alitokea na kutembea pamoja nao.

Mara macho yao yalipofunguliwa, wale wafuasi wawili walikimbia kwenda Yerusalemu kushiriki mambo yaliyowatokea njiani (Luka 24:33—35). Yesu alipokuja na kusimama katikati yao, waliogopa sana. Tazama maswali Yake kwao: “ ‘Mbona mnafadhaika: Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu?’ ” (Luka 24:38). ;

Huu ni ujumbe wa Yesu kwetu leo pia: Mara nyingi tunasahau kwamba Yeye anatembea pamoja nasi katika mabonde yetu. Mara nyingi hatumtambui. Mara nyingi tunasahau kwamba kuna mengi zaidi katika kisa. Mara nyingi tunasumbuka na kuruhusu mashaka kujaa mioyoni mwetu, tukisahau kwamba Yesu anashikilia maisha yetu pasi na hofu mikononi Mwake. Na mara nyingi tunadhani tunajua zaidi kuliko Yesu kuhusu kile kinachoendelea katika maisha yetu (Luka 24:18).