HomeResourcesSabbath School quarterly

Imanueli, Mungu Pamoja Nasi

09/04/2026

Kama ungekuwa unaangalia namna ya kumshirikisha mtu asiye Mkristo maelezo ya tabia ya Mungu kutoka katika Biblia, ungefungua wapi?

Kwa kweli, jibu zuri kuliko yote, lingekuwa ni Yesu. Biblia inasema kwamba Bwana Yesu hamwakisi tu Mungu bali pia anamfunua Mungu. Kuna vifungu vingi vya Biblia vinavyolielezea hili, lakini kimoja kinachofanya hili kwa usahili sana ni Yohana 14:9. Hapa, Bwana Yesu anasema, “Aliyeniona mimi amemwona Baba.” Ili tupate kujua zaidi kuwa Mungu yukoje, yatupasa kumtazama Yesu — maneno Yake, matendo Yake, namna Yake ya kufanya mambo, na upendo Wake mkuu kwa wanadamu katika kifo na ufufuo Wake.

Upendo na uangalizi wa Baba unaelezewa kwa namna iliyo wazi zaidi katika Mwana Wake, Yesu. Uzuri wa Biblia ni kwamba Mungu ametupatia mitazamo minne iliyosheheni sana ya maisha ya Yesu ili tupate kuwa na picha kamili inayomwonesha Mungu kuwa ni nani. Kwenye Mathayo (ikiwa imeandikwa na Myahudi, kwa ajili ya Wayahudi), tunamwona Yesu kama Masihi aliyesubiriwa sana ambaye alitimiza kile kilichokuwa kimeahidiwa. Kwenye Marko, tunamwona Yesu akiishi maisha ya utendaji ya huduma na kujitoa. Daima alikuwa akiwafikiria wengine na daima akiitikia mapenzi ya Baba Yake. Kwenye kitabu cha Luka, tunaweza kusoma juu ya namna Yesu alivyojisikia, akiwa na rehema na ubinadamu Wake mkamilifu, nasi tunaweza kusoma kisa hiki ili kuwa na uhakika kwamba kile tunachokisoma ni kweli (Luka 1:3, 4). Kwenye Yohana, tunamwona huyu Mwana wa Mungu aliyefanyika mwanadamu nasi tunakaribishwa kuamini kwamba Yesu ndiye Yule anayedai kuwa hivyo, ili maisha yetu ya kiroho yapate kuhuishwa. Ingawa vitabu vyote vinne vya Injili vinachungua eneo hilo hilo, “haviwasilishi mambo kwa mtindo mmoja tu. Kila mwandishi ana uzoefu wake mwenyewe, na utofauti huu unapanua na kuongeza ujuzi unaotolewa ili kukidhi mahitaji ya watu wenye mawazo mbalimbali.” — Ellen G. White, Manuscript 105, 1900. Ni Injili gani ambayo umeisoma hivi karibuni zaidi?

Tumegusa juu juu tu katika mada hii kubwa, tabia ya Mungu. Mungu ni mkuu na wa ajabu kuliko tunavyoweza kuelewa, na tutakuwa tukijifunza juu yake milele.