HomeResourcesSabbath School quarterly
Nipe tu Ishara
17/05/2026
Huenda umewahi kusikia watu wakisema, Kama tu ningeweza kuona bahari ya Shamu ikigawanyika, au mana ardhini, au Yesu akimponya kipofu, ningeamini. Au bila shaka wewe mwenyewe umewahi kuwa na fikra za jinsi hiyo.
Kwa nini iwe rahisi kwetu sasa kuwa na imani kuliko ilivyokuwa kwa wale wa zama za kale za Biblia? Waisraeli hawakuwa na Biblia nzima, wala hawakuwa na historia ndefu ya kurejelea kama ilivyo kwetu. Musa alihimiza juu ya umuhimu wa kurejelea historia ili kukumbuka uongozi na wema wa Mungu (taz. Kum. 4:7-10; Kum. 8:2,3). Tofauti na Waisraeli, tuna miaka 6,000 ya historia ya Biblia ya kurejelea (taz. Yohana 20:30, 31).
Kila kizazi kinataka ishara, na cha kwetu hakina tofauti. Lakini ishara zimetuzunguka pande zote. Ikiwa utasoma Mathayo 24, utaona ni vitu vingi kiasi gani vimetimia na vinatimia hata sasa.
Je, tunabishana na Yesu na kumjaribu kama walivyofanya Mafarisayo? Je, tunamfanya augue sana rohoni mwake(Marko 8:12) kwa sababu ya kukosa imani kwetu wakati ambapo tayari ametupatia vyote tunavyohitaji ili kuamini? Lakini ishara hizi hazikuwa hasa walichohitaji. Hakuna ushahidi wowote wa nje ambao ungewafaa. Walichohitaji hakikuwa kuangaziwa kiakili, bali matengenezo ya kiroho. —Ellen G. White, Tumaini la Vizazi Vyote-Sehemu ya pili, uk. 12. Je, yumkini sisi pia tunahitaji matengenezo ya kiroho, matembezi ya dhati, halisi na ya daima pamoja na Mungu? Bila shaka, kiukweli hatuhitaji ishara, kwa sababu tunao utitiri wa maarifa mikononi mwetu, hasa kutoka katika Biblia.
Hivyo, badala ya kumfanya Yesu (augue) sana kwa sababu ya kukosa imani kwetu, hebu tukumbuke maneno ambayo Yesu alisema kwa Thomaso: wa heri wale wasioona, wakasadiki (Yn. 20:29; taz. pia Ebr. 11:1). Mungu hatuombi kuwa na imani isiyoona — tayari Ametupatia utitiri wa sababu za kuamini. Na bado pamoja na wingi huu wote wa sababu, daima kuna fursa ya kuona shaka. Cha msingi ni kulenga katika kila kinachoithibitisha imani na wala si kwa kile kiletacho mashaka.