HomeResourcesSabbath School quarterly
Mifano ya Imani
20/05/2026
Tumia muda leo kujifunza Waebrania 11, sura ya imani kuu. Isome kwa sauti kwanza bila kukoma. Kisha soma mara ya pili, na uandike mawazo yako kutokana na maswali haya:
- Soma tena aya ya kwanza. Ni kitu gani unakitarajia leo ambacho bado huwezi ona? (Fikiria juu ya mahitaji ya haraka na njozi za muda mrefu.)
- Je, imani ina sehemu gani katika ushuhuda wako binafsi na katika uongofu wako?
- Soma aya 3 tena, juu ya Mungu na uumbaji. Kwa nini, kwa namna nyingi, kuwepo kwa Mungu Muumbaji kiwe kitu rahisi kukubali kwa imani?
- Soma aya ya 6 na uandike ujumbe wa aya hii kwa maneno yako mwenyewe.
- Aya za 7-40 zinafunua maisha ya wahusika mbalimbali wa Kibiblia. Kwa nini imani ni kipengele kikuu ambacho kinafasili uimara wa uhusiano wa watu hawa na Mungu?
Kumjua Mungu na kuwa na uhusiano hai na imara Naye kunahitaji —imani. Unawezaje kuimarisha imani yako au kumtia shime mtu ambaye imani yake inayumba? Hapa kuna mawazo machache:
Imani ndogo kabisa (kama punje ya haradali) ina nguvu na ndiyo unayohitaji ili kujenga uhusiano na Mungu (Mt. 17:20). Ili mradi uko tayari kufanya kazi Naye, Mungu atasaidia imani yako kukua.
Imani huja kwa kumsikia Mungu akizungumza nasi katika Neno lake, Biblia (Rum. 10:17). Azimia kujifunza Biblia na kuomba kila siku.
Mwombe Mungu akuongezee imani(Luka 17:5). Kama alivyofanya yule baba aliyekuja kwa Yesu akiwa na mtoto aliyepagawa na pepo na ambaye alipaza sauti, akasema “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9:24) tunaweza kutambua kutokuamini kwetu na kumwomba Mungu atuongezee imani yetu.
Imani na mashaka vinaweza kukaa pamoja (Marko 9:24). Usimwache Mungu kwa vile tu una maswali. Kwa kweli, ni muhimu kushughulikia wokovu wako kwa kicho na kutetemeka (Wafilipi 2:12-16) na kumilikiimani yako kuliko kuazima kutoka kwa mwingine kama wale wanawali watano walivyojaribu kufanya (Mt. 25:8).
Mwitikie Roho Mtakatifu na uombe ujazo wake zaidi katika maisha yako.
Tumia imani yako. Kumbuka kuwa imani sio hisia bali uamuzi wa kuamini. Kumbuka kuwa hata gizani, wakati usipoweza kumwona, Mungu yupo (2 Kor. 5:7).
Kama ombi binafsi la shukrani kwa Mungu kwa uaminifu Wake, angalia maneno ya wimbo Kweli U Mwaminifu.(KK. 30)