HomeResourcesSabbath School quarterly
Toba na Msamaha
30/05/2026
Somo la Juma Hili
Isa. 61:10; Hos. 6; Mdo. 3:18, 19; Kut. 34:1-10; Rum. 6:23; Mt. 22:1-14.
Fungu la Kukariri
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote(#1 Yohana 1:9#).
Nchi, ya Ahadi ilionekana kuwa mbali sana kwa Waisraeli, waliokuwa wamepiga kambi chini ya nguzo ya wingu katika uwanda. Musa alikuwa amepanda katika giza nene, lililokuwa limefunika kilele cha mlima siku nyingi zilizopita. Bila shaka kiongozi wao alikuwa amekufa sasa, walifikiri, ikiwa si kwa kukosa chakula basi huenda kwa moto ulao juu ya kilele. Kundi hili mchanganyiko (Waisraeli pamoja na wale walioondoka Misri pamoja nao wakati wa Kutoka) walihisi wasiwasi na kukosa uvumilivu, wakiwa tayari kusonga mbele kuelekea nchi inayotiririka maziwa na asali. Ingawa watu hao hao walikuwa, siku chache tu nyuma, wamefanya agano la dhati na Mungu la kumtii, walitaka sanamu ambayo wangeweza kuiona. Hivyo, wakakusanyika karibu na hema ya Haruni na kumtaka awatengenezee sanamu. Kwa kuhofia usalama wake mwenyewe, Haruni alikubali. Katika Kutoka 32-34, tunasoma jinsi kisa hiki cha kusikitisha kinavyojifunua.
Simulizi hii ni kisa kutoka katika Maandiko kinachotufundisha kuhusu toba na msamaha, mada ya somo la juma hili. Weka mada ya somo la juma hili akilini unapopitia masomo ya kila siku. Ni kweli, tunatenda dhambi, lakini kwa sababu ya kifo cha Yesu msalabani, msamaha upo kwa mwenye dhambi anayekiri kwa dhati na kutubu.
Jifunze somo la juma hili ukijiandaa kwa Sabato, Juni 6.