HomeResourcesSabbath School quarterly

Vazi la Gharama Kubwa Kabisa

04/06/2026

Mavazi mazuri mara nyingi huashiria utajiri kwa viwango vya kidunia. Watu wengine husema, “Ninavaa hivi ili kuonesha mimi ni nani.” Lakini mbinguni, kila kitu isipokuwa mahusiano yetu kitapotea (Mathayo 6:19-21). Utambulisho wetu binafsi unapaswa kufunikwa na Yesu na vazi Lake kamilifu la haki.

Yesu alimwita yule mtu asiye na vazi rafiki, na licha ya kutokuitikia kwake, ni wazi walikuwa na uhusiano kabla ya hapo. Mtu huyo lazima alikuwa akijua kuhusu lile vazi, lakini alichagua kutolivaa. Tabia ya Yesu ni kamilifu na isiyo na waa, naye hutupatia ili kanisa Lake “kuvikwa kitani nzuri, ing'arayo, safi” (Ufunuo 19:8), lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo(Waefeso 5:27).

Kitani nyeupe “ni haki ya Kristo, tabia Yake isiyo na waa, ambayo kwa imani wanapewa wote wanaompokea kama Mwokozi wao binafsi,” —Ellen G. White, Christs Object Lessons, uk. 310.

Adamu na Hawa walivaa vazi jeupe la nuru tulivu kabla hawajatenda dhambi; baada ya kutenda dhambi, walitambua kuwa walikuwa uchi (Mwa. 3:7) nao wakajitengenezea mavazi ya majani ya mtini. Kisha Mungu akabadilisha mavazi yao ya majani ya mtini kwa mavazi ya ngozi ya mnyama. Kulikuwa na dhabihu iliyosababisha vazi lao. Kwa namna hiyo hiyo, tunapokea dhabihu ya Yesu kwa kukubali vazi Lake la haki. Wakiwa uchi na wenye aibu, walijaribu kuchukua nafasi ya mavazi ya mbinguni kwa kushona pamoja majani ya mtini kwa ajili ya kujifunika... . Hakuna kitu ambacho mwanadamu anaweza kubuni kuchukua nafasi ya vazi lake la kutokuwa na hatia lililopotea. Si vazi la majani ya mtini, si mavazi ya watu wa kidunia, yanayoweza kuvaliwa na wale wanaoketi pamoja na Kristo na malaika katika karamu ya harusi ya Mwanakondoo. Ni vazi tu ambalo Kristo Mwenyewe amelitoa ndilo linaloweza kutufanya tufae kuonekana mbele za Mungu. Vazi hili, vazi la haki Yake Mwenyewe, Kristo ataivika kila roho inayotubu na kuamini.—Ellen G. White, Christs Object Lessons, uk. 311.