HomeResourcesSabbath School quarterly
Pasipo Kulazimishwa lakini kwa Nguvu
15/06/2026
Je, umewahi kujiuliza ni kwa jinsi gani Yesu aliweza kudumisha motisha ya kufanya kazi, kuponya, kufariji, kuhubiri, na kufundisha watu wengi siku baada ya siku? Tunaambiwa kwamba “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji” (Mathayo 9:36). Upendo na huruma za Yesu kwa wanadamu ndivyo vilivyomsukuma kutenda. Vivyo hivyo, upendo wa Mungu ndani yetu unapaswa kutusukuma kuhisi mzigo wa kuwaongoza watu Kwake na kwa kweli Yake (2 Wakorintho 5:14).
Je, umewahi kutazama nyuso za watu usiowajua katika kutaniko la watu na kufikiri kuhusu umilele, ukijiuliza kama wanamjua Yesu? Je, umewahi kuhisi kile kinachoweza tu kuwa upendo wa Mungu ndani yako kwa mtu usiyemjua mwenye uhitaji? Upendo wa Mungu ndani yetu hutusukuma kuhisi mzigo wa kuwaongoza watu Kwake. Yeremia alieleza hili aliposema, “Ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia” (Yer. 20:9).
Hata hivyo, tunapomshuhudia Mungu kwa wengine, kamwe hatupaswi kumlazimisha mtu kumpokea Mungu au ukweli Wake wa Biblia. Kulazimisha kunapingana na kiini cha tabia ya Mungu. Mungu hakuwalazimisha Adamu na Hawa kujitenga na mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Mwanzo 2:16, 17). Hakuwalazimisha watu kuingia ndani ya safina ili waokoke dhidi ya Gharika Mwanzo 7:1. Hakuwalazimisha Waisraeli kudumu Katika agano lao pamoja naye (Kum. 4:29-31). Badala yake, Aliwatimizia mahitaji yao (Mathayo 4:23-25) na kisha akawaalika kumfuata. Yesu hakumlazimisha mtu yeyote kumfuata Yeye wala ukweli Wake, lakini kamwe hatukatii tamaa (Mathayo 23:37).
Tunaposhuhudia, mbinu yetu inapaswa kila wakati kuakisi mbinu ya Yesu. Ellen G. White anasema, “Si sehemu ya utume wa Kristo kuwalazimisha watu wampokee, Ni Shetani, na watu wanaoongozwa na roho yake, wanaotafuta kulazimisha dhamiri. .... Hakuna ushahidi wa wazi zaidi kwamba tunayo roho ya Shetani kuliko tabia ya kuumiza na kuharibu wale wasiothamini kazi yetu, au wanaotenda kinyume na mawazo yetu.”—TheDesire 0 Ages, 487
Tunapaswa kujiruhusu kuwa vyombo vya huduma ya Mungu. Tunaishi, katika dunia inayochukia ukweli, lakini uhalisia huo haupaswi kutuzuia kushiriki kwa njia ya busara na ya upendo. Kumbuka kwamba mara nyingi ushuhuda wetu binafsi ndio unaobeba uzito mkubwa, hasa katika hatua za awali za kushuhudia (Ufu 12:11).