HomeResourcesSabbath School quarterly
Vidokezo kwa Ajili ya Kumshuhudia Yesu
16/06/2026
Swali kwa kila mmoja wetu ni hili: Unamshuhudia Yesu kwa nani—mchukuzi wa posta, mwuzaji dukani, mtu unayemwona kila siku unapokuwa ukitembea? Mungu anamwita kila muumini kushiriki katika kazi hii, na anaahidi kukupa “ ‘ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka’ ” (Isaya 50:4). Ni wajibu pia wa Mkristo kuwa tayari kila wakati kutoa utetezi (apologia) kwa ajili ya imani na tumaini Lililo ndani yetu (1 Petro 3:15).
Vifuatavyo ni baadhi ya vidokezo rahisi vya kuzingatia unapotafakari jinsi ya kudhamiria katika kumshuhudia Yesu kwa wengine:
- Mfahamu mtu na ujenge urafiki naye kwa muda. Wema, huruma, na nia ya kweli juu yake (kuwa “wa kupendeka”) vitamsaidia kuvutwa kwa Mungu. (Wengine huiita hili “uinjilisti wa urafiki.”)
- Omba Roho Mtakatifu afanye kazi katika moyo wa mtu huyo. Omba kwa ajili ya fursa sahihi za kuwasiliana naye.
- Tafuta njia za kawaida za kuzungumza kuhusu uzoefu wako wa imani au kumwombea. Mwombe Mungu akupe ujasiri lakini pia upole katika mbinu yako.
- Tafuta njia za kumuunganisha rafiki yako mpya pamoja na wengine kutoka kanisani kwako, ili aweze kupata fursa ya kuingia katika jamii ya waumini. Kikundi kidogo cha kijamii au cha kujifunza Biblia ni hatua nzuri inayofuata. Ombea mahitaji maalum au maswali ambayo rafiki yako mpya anaweza kuwa nayo, na tafuta fursa ya kumwonesha jinsi Biblia inavyotoa faraja, ushauri, na mwongozo katika maisha yetu. Unaweza kuanza kwa kushiriki ahadi moja ya Biblia au kujibu swali moja, jambo ambalo linaweza kufungua mlango wa majadiliano ya kina zaidi. Yaombee pia.
- Utafika wakati ambao utatakiwa kumwuliza rafiki kama angependa kuchukua hatua inayofuata (kujifunza Biblia na, hatimaye, ubatizo). Usiharakishe hatua hizi, lakini pia usichelewe. Omba kwa ajili ya hili.
- Matendo yetu yanapaswa kumfunua mmiliki wetu. Jinsi tunavyowatendea wengine katika maisha yetu itaonekana. Tabia zetu zinapoumbwa kufanana naye (kutakaswa), tutaishi kwa namna inayowavuta watu wote Kwake.